22.11.13

Monday, October 07, 2013

(News) Watanzania walia na kodi laini ya simu

·        Wasema kodi ya shilingi 1,000/- ya laini ya simu ya kila mwezi hailipiki

Dar es Salaam, 7 Septemba 2013 … Asilimia 99 ya watanzania ambao wametoa maoni yao kuhusu ya kodi mpya ya shilingi 1,000/- kwa laini ya simu kila mwezi, wamesema kodi hiyo haiendani na uwezo wa kifedha wa watumiaji wa simu, asilimia 0.6 wamesema ni sahihi kutozwa kodi hiyo wakati asilimia 0.1 hawakuwa na upande wowote.

Kipindi cha utoaji wa maoni ya tozo hiyo kiliendeshwa na kituo cha ITV  na Radio One Alhamisi Oktoba 3,na ijumaa Oktoba 4 ambapo watumiaji wa simu zaidi ya 510,000 wa mitandao ya Tigo,Vodacom na Airtel, walisema  kodi hii sio sahihi kwa kuwa watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini tayari wanalipa asilimia 14.5 ya matumizi yao ya simu kama kodi.


Aidha, waliotoa maoni yao kuhusu kodi hiyo, waliishauri serikali kutafuta vyanzo mbadala vya mapato badala ya kuwatwisha mzigo mkubwa wa kodiwatumiaji wa simu nchini kwani tayari wanalipa kodi nyingine  zinazotokana na matumizi ya huduma hiyo.

Hivi karibuni makampuni yanayotoa huduma za simu za mkononi nchini yalifungua kesi katika mahakama inayoshughulika na masuala ya kodi kutaka kodi hiyo isimamishwe. Makampuni hayo ambayo ni wanachama wa Muungano  wa makampuni yanayotoa huduma za simu za mkononi  (MOAT) ni Tigo, Airtel,Zantel,Vodacom Tanzania na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Makampuni ya simu mwezi uliopita yalitakiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kulipa limbikizo la kodi ya laini ya simu kuanzia mwezi Julai ambapo utozwaji wa kodi hiyo ulipaswa kuanza hadi mwezi Septemba, ambapo kampuni inapaswa kulipa shilingi 3,000 kwa kila laini ya simu ya mteja wake na fedha hizo zinapaswa kukatwa kwa wateja wa makampuni yaani watumiaji wa simu.

Taarifa za hivi karibuni zilizotolewa na makampuni ya simu zilibainisha kuwa watumiaji wa simu za mkononi wapatao milioni 8 wanatumia chini ya shilingi 1,000 kwa mwezi na hawana uwezo wa kulipa kodi ya laini ya kilawezi na watakatiwa mawasiliano endapo utekelezaji wa tozo ya laini utakapoanza.

Aidha, mnamo tarehe Julai 23, Rais Jakaya kikwete aliagiza iundwe kamati ya wadau wote ili kuangalia upya suala hili la kodi ya laini ya simu na aliwataka wadau hao wakae pamoja na kuangalia ni jinsi gani serikali ingeweza kuziba pengo la kodi iliyotarajiwa kukusanywa kutokana na tozo hiyo iwapo tozo hiyo ingesitishwa.

Vyanzo kadhaa vya kuaminika vimeeleza kwamba makampuni ya simu yaliwasilisha mapendekezo yao ambayo hadi sasa hayajawekwa wazi. Tangu kutangazwa kwa tozo hii, umoja wa makampuni ya simu za mkononi nchini umekuwa ukiomba kuondolewa kwa kodi hii kwa wateja wake kwa kuwa,  licha ya  kuelewa lengo zuri la serikali la kukusanya fedha kwa ajili ya maendeleo ya nchi kupitia kodi hii, utekelezwaji wake utawaumiza wananchi wa kipato cha chini.

Tofauti na kodi nyingine zinazotozwa kulinga na kipato cha mtumiaji, kodi hii haizingatii uwezo wa walengwa na itatozwa kwa wote. Sekta ya mawasiliano inatarajia wateja wake wapya wa siku za usoni watatoka vijijini lakini kodi hii itawaumiza watumiaji  hao hao kwani itawaongezea mzigo mkubwa wa kodi wakazi wa maeneo hayo na hivyo kukinzana na dhamira ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora ya mawasiliano kupitia simu za mkononi.

No comments: