22.11.13

Tuesday, September 07, 2010

ALLIANCE FRANCEE WATANGAZA MICHONGO KWA WASANII

Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Utamaduni cha Ufaransa, Didier Martin (Katikati) akiwasilisha mada yake iliyohusu Mchango wa Asasi kama yake Kwenye kukuza Sanaa na Utamaduni wa Mtanzania.Kushoto kwake ni Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego na Ruyembe Mulimba.

Msanii wa Kizazi kipya Symon John aka Gheto King akichangia hoja kwenye Jukwaa la Sanaa.

‘Saidieni jamani Sanaa Yetu Ikue’ ndivyo Mzee Rashid Masimbi ambaye ni Mtaalamu wa Sanaa za Maonyesho alivyokuwa akitoa mchango wake kwenye Jukwaa la Sanaa Jumatatu hii.

Sehemu ya wadau wa Jukwaa la Sanaa wakifuatilia kwa makini wasilisho la Mkurugenzi wa Alliance Francee,Didier Martin.

Mkongwe wa Muziki wa Dansi, Hussein Jumbe yeye alitaka aelezwe ni kwa Jinsi gani ataweza kushiriki Tamasha la Sauti za Busara ambalo limekuwa likidhaminiwa pia na kituo hicho.

Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego (Kushoto) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa Alliance Francee, Didier Martin muda mfupi baada ya kuliahirisha Jukwaa la Sanaa hadi Jumatatu ijayo ambapo Mada kuhusu Changamoto za Sanaa ya Unenguaji Itawasilishwa.

Kituo cha Kimataifa cha Utamaduni cha Ufaransa (Alliance Francee) kimewataka wasanii wa Bongo kutumia programu yake ya Barazani katika kutangaza kazi zao na kuzifanya zitambulike na kupata soko kimataifa.
Barazani ni programu ya ‘pafomansi’ za kisanaa ambayo imekuwa ikiwahusisha wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi na imekuwa ikifanyika kwa mwezi mara moja kwenye kituo hicho cha utamaduni.Mwezi huu itafanyika Tarehe 15.

Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwa kuandaliwa na BASATA likishirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz),Mkurugenzi wa Kituo hicho BW.Didier Martin alisema kwamba, wasanii hawana budi kulitumia jukwaa hilo katika kuuza na kutambulisha kazi zao kwani limekuwa likihudhuriwa na watu mbalimbali kutoka sehemu tofauti duniani.

Alisema kwamba, ushiriki wa wasanii kwenye jukwaa hilo uko wazi kinachotakiwa ni wasanii wenyewe kuchangamkia fursa hiyo kwa kufika kwenye kituo hicho na kujiandikisha.

Aidha, alisema kwamba, kwa sasa kituo hicho kinatoa mafunzo ya lugha ya Kifaransa kwa watu mbalimbali na kuongeza kwamba, gharama za malipo zimepunguzwa kwa wasanii hadi kwa zaidi ya asilimia hamsini hivyo ni fursa pekee kwa wasanii kujifuna lugha hiyo ya kigeni.

Kuhusu nyimbo za wasanii wa muziki kusikika redioni,alisema kwamba, Ufaransa imefungua kituo cha redio ambacho kitarusha matangazo kwa lugha ya Kiswahili na kuongeza kwamba, mwezi ujao wanatazamia kuanzisha dawati la Kiswahili.Bila shaka wasanii wanaobanwa kwenye ‘ea taim’ watumie fursa hiyo.

Masuala ya msingi yaliyojadiliwa kwenye jukwa la sanaa Jumatatu hii na wadau wengi ni pamoja na haja ya kituo cha Alliance Francee kupenya hadi vijijini, kusaidia kuhamasisha wawekezaji wa Kifaransa kujenga studio za kurekodia nchini, kusaidia usambazaji wa kazi za wasanii,kutoa msaada wa kifedha kwa wasanii nchin, kuzitangaza kazi za wasanii wa ndani nje ya miapaka nk.

Akijibu masuala hayo, Mkurugenzi Martin alisema kwamba, kwa sasa kituo chake kinatoa msaada wa fedha kwa wasanii wanaofanya sanaa zenye uasili wa Tanzania na kusisitiza kwamba, wasanii wa Tanzania lazima waachane na dhana ya kunakiri kazi kutoka nje bali wajikite kwenye kutengeneza kazi za sanaa za asili.

Aliongeza kwamba, tatizo la masoko ya kazi za Sanaa ni kubwa lakini akasisitiza kwamba, wasanii wanapaswa kujikita kwenye ubunifu wa kazi zilizo bora na zenye kubeba asili ya Tanzania ili kuzifanya kuwa tofauti na zile zinazotolewa sehemu zingine duniani.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonce Materego alisema kwamba, Baraza lake litaendelea na utaratibu wa kuwapa wasanii fursa mbalimbali za kukutana na wadau wa sanaa wa ndani na nje hata hivyo naye akakumbusha kitu ambacho ambacho muda wote amekuwa akikisisitiza cha wasanii wetu kubuni kazi zenye asili ya kwetu.

Alisema kwamba, kunakiri kila kitu kutoka nje maana yake ni kudumaza sanaa yetu na hivyo kuwafanya wasanii kushindwa kushindana kwenye masoko kutokana na kutengezeza kazi zinazopatikana kwingineko duniani.

No comments: