Mnenguaji wa Bendi ya Extra Bongo, Husna akichangia mada.Aliomba panga la BASATA liwakate wale wanaovaa nusu uchi tu kwani baadhi yao hawavai hivyo.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka viongozi wa Bendi kuacha mara moja tabia ya kuwadhalilisha wacheza shoo (wanenguaji) kwa kuwavalisha mavazi ya kutia aibu na yanayodhalilisha utu wao.
Aidha,BASATA imewataka wanenguaji hao kuthamini utu wao na kufikiria upya dhana kwamba bila kuvaa nusu uchi basi sanaa ya muziki wa dansi haiwezi kupata soko na kuvutia watazamaji wengi kwenye maonyesho.
Akizungumza kwenye Jukwaa la Sanaa linaloandaliwa kwa pamoja na BASATA na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz) na kufanyika kila Jumatatu,Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alisema kwamba, lazima wadau wa muziki wa dansi wafikirie upya na kubadili mara moja tabia ya kuendekeza maonyesho yanayochafua maadili ya mtanzania.
“Wanenguaji lazima wafikie hatua waseme kwamba, udhalili wa nusu uchi basi tena.Wavae mavazi yenye heshima kama wanavyovaa wale wa kiume” alisema.
Aliongeza kuwa dhana kwamba bila wanenguaji kuvaa nusu uchi maonyesho ya muziki wa dansi hayapati watazamaji na biashara haifanyiki ni uongo na inaonesha jinsi wasanii wa dansi walivyokosa ubunifu wa kuvutia watu kwenye maonyesho yao na badala yake kubaki wakiendeshwa na hisia zisizo za kisanaa.
“Ushindani wa kibiashara ambao unaomfanya msanii kuwa dhalili ili kuvuta watu kwenye maonyesho haukubaliki bali unawafanya wasanii kuwa makapuku na wanaopoteza thamani yao” aliongeza.
Alisisitiza kwamba, BASATA limekuwa likikemea na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya unenguaji wa nusu uchi lakini mabadiliko yamekuwa ni ya muda na baadaye kurudi kwenye udhalilishaji uleule.
Aliongeza kwamba,Baraza kwa sasa linafanya utafiti kwenye sanaa ya unenguaji na mara utakapokamilika mwongozo kwenye sanaa hii utatolewa na kutakiwa kufuatwa na wadau wote.
Kwa upande wake, mwasilishaji wa mada Mama Nsao Shalua ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji sanaa, BASATA alisema kwamba, mavazi katika kazi ya sanaa yapo kwa ajili ya kuwakilisha tamaduni za jamii husika hivyo vichupi vinavyoonekana kwenye majukwaa yetu havina utambulisho wala maana yoyote.
‘Maleba (mapambo/mavazi) katika sanaa yoyote yanakuwa na utambulisho wa jamii na kazi husika hivyo vivazi vya nusu uchi vinavyovaliwa havina nafasi” alisema.
Katika Jukwaa hilo la sanaa lililopambwa na maonyesho ya wanenguaji kutoka bendi mbalimbali nchini waliokuwa katika mavazi tofautitofauti wadau wengi walilamika juu ya mavazi ya kutia aibu wanayovaa wanenguaji na kutoa wito wa hali hiyo kukoma mara moja.
Jukwaa la Sanaa litaendelea kama kawaida Jumatatu ya wiki ijayo kwenye Ukumbi wa BASATA ambapo mada itakuwa ni Soko la Ubunifu wa Mavazi Tanzania na Changamoto zinazowakabili itakayowasilishwa na Mbunifu maarufu nchini Mustapha Hassanali.
Habari/Picha na Afisa Habari wa BASATA,
Alistide Kwizela
No comments:
Post a Comment