22.11.13

Saturday, February 11, 2012

TAMASHA LA SAUTI ZA BUSARA.

 Tamasha la Sauti za Busara limeng’oa nanga kwa staili ya aina yake kwa ngoma za asili kama Mdundiko, Ngongoti,  Dufu na shangwe katika maandamano maarufu kama Carnival Parade  ambayo yalianzia Kisonge Park saa kumi kamili jioni na kuishia   Ngome Kongwe saa kumi na mbili jioni.
Vitongoji mbalimbali Unguja vilipata bahati ya kujionea maandamano hayo kwani msafara huo ulikatiza katika vitongoji vya Michenzani,Kisiwandui,Mkunazini, Mnazi mmoja, Maisara,Mnazi Mmoja, Vuga na Shanghani kabla ya kutia nanga Ngome Kongwe.
Baada ya hapo siku nne za burudani na muziki mfululizo katika visiwa vya Unguja zimeanza rasmi.Vikundi saba vimetoa burudani ndani ya viwanja vya Ngome Kongwe,  ambavyo  ni Mkota Spirit Dancers kutoka  Pemba, Swahili Vibes, Shirikisho Sanaa, Tandaa Traditional Group, Wanafunzi wa SOS, Ary Morais (Cape Verde/Norway) na Mashauzi Classic modern taarab ya Tanzania ikiongozwa na Isha Mashauzi.
Kikundi kutoka Pemba,Mkota Spirit Dance kilifanya shoo ya aina yake  iliyopambwa na uvaaji na nyimbo zao za Kiswahili cha aina yake kama Uganga Ukuu, Ng’ombe alia Baa, Ukaruka Mgongowa na Bamba la Mvumo.
Jike la Simba, Isha Mashauzi  aliwarusha wakazi na wageni kwa uimbaji wake na uchezaji wa nyimbo zake maarufu kama Mama Nipe Radhi na Tugawane Ustaarabu ambazo ziliwafanya hata wasioelewa alichokuwa akiimba walivuja jasho kutokana na kucheza mwanzo mwisho.


 Pamoja na muziki kutoka katika vikundi mbalimbali, katika viunga vya Ngome Kongwe, vinaonyeshwa vipande vya video za aina mbalimbali ya muziki kama vile Taarab, Kuduro, Hip Hop, Bongo Flava, Mchiriku  na hili litakuwa likifanyika kila siku.
Tayari wanahabari wa ndani na wakimataifa, mameneja wa wanamuziki na wadau mbalimbali wa sanaa, wameanza kukutana na kubadilishana uzoefu katika Movers & Shakers. Wenyeji wanapata nafasi ya kujifunza, kutokana na habari za mafanikio kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Bado tunaendelea  kulifanya tamasha kuwa  la kila Mtanzania  ambalo anaweza kuingia na kushuhudia burudani.  Watanzania wanaingia bure mpaka saa 11.30 jioni, baada ya hapo atalipa shilingi 3000, mkazi wa Afrika Mashariki atalipa dola 7 na kwa wageni kutoka mataifa mengine watalipa dola 26.
Tamasha la Sauti  2012 linafadhiliwa na The Norwegian Embassy, HIVOS, Mimeta, Roskilde Festival Charity4 Society, Grand Malt, Toyota, CBA, Goethe Institut, US Embassy, African Leisure Centre, fly540, Memories, Zanlink, Azam Marine, SMOLE II, Zanzibar Grand Palace Hotel, Maru Maru Hotel, Embassy of France, Tabasam Tours, Times FM Radio, fROOTS, Ultimate Security

Kwa habari zaidi tembelea   www.busaramusic.org 

No comments: