22.11.13

Tuesday, June 12, 2012

WASANII JIPANGENI KUHIMILI USHINDANI WA KIMATAIFA

Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego akisisitiza jambo wakati akihitimisha mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya BASATA.Wengine kulia ni Mhandishi Joel Chacha kutoka malaka ya mawasiliano nchini (Tcra) na Kaimu Mratibu wa Jukwaa hilo Agnes Kimwaga.

Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii kujipanga kwa ajili ya kuhimili ushindani wa kimataifa kutokana na ujio wa mfumo wa digitali ambao utazifanya kazi zao kuonekana kimataifa.

Wito huo umetolewa wiki hii kwenye ukumbi wa BASATA na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Ghonche Materego wakati akihitimisha mjadala kwenye Jukwaa la Sanaa uliohusu Teknolojia ya Digital na Faida Zake Katika Sekta ya Sanaa uliochokozwa na Mhandisi Joel Chacha kutoka mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (Tcra).

Alisema kuwa, mfumo wa digitali utaruhusu uwepo wa vituo vingi vya redio na runinga ambavyo vitakuwa na masafa ya kimataifa hivyo ni wazi wasanii wanatakiwa kujipanga katika kuandaa maudhui bora, ya kutosha na yenye mvuto kwa ajili ya kukidhi ongezeko hilo na zaidi ushindani wa kimataifa.

“Wasanii tujipange, fursa zinazokuja ni nyingi mno, zinahitaji maudhui ya kutosha, yenye ubora na yatakayoweza kuvifanya vyombo vya habari viweze kuhimili ushindani pia” alisisitiza Materego.
Aliongeza kuwa, moja ya eneo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wamiliki wa vyombo vya habari ni uhafifu wa maudhui ya kazi za Sanaa hivyo, wasanii hawana budi kuacha kulalamika na kujipanga kukabili changamoto hiyo.
Awali akiwasilisha mada hiyo,Mhandisi Chacha alisema kuwa, mfumo wa digitali utazalisha fursa nyingi katika sekta ya Sanaa lakini akasisitiza kuwa, uchangamfu wa Wasanii wetu ndiyo utawafanya wafaidi.
Alizitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na; ongezeko la ajira kwa Wasanii, ongezeko la vipindi, kukua kwa ushindani katika ubunifu na utengenezaji maudhui yenye ubora, Sanaa za Tanzania kutangazika kimataifa na kuongezeka kwa makampuni yatakayojihusisha na sekta ya Sanaa

“Mfumo wa digitali una mazuri mengi lakini kubwa ni kuongezeka ushindani na ubora katika kutengeneza maudhui yenye ubora na pia ongezeko la masafa katika televisheni ambayo yatahitaji maudhui (vipindi) ya kutosha” Aliongeza Chacha.

Hata hivyo, aliitaja changamoto ya uharamia kwenye sekta ya Sanaa ambapo aliwashaiuri wasanii kuamka na kujiunga na Chama cha hakimiliki (Cosota) ili kuhakikisha kazi zao zinalindwa kisheria.

Wadau wengi waliochangia mjadala huo walionekana kuwa na wasiwasi na mfumo wa digitali lakini wakaomba elimu ya kutosha itolewe ili wananchi wengi zaidi waelewe nini maana ya kutoka mfumo wa analogia kwenga ule wa digitali

No comments: