22.11.13

Tuesday, August 07, 2012

BASATA LAKERWA NA WASANII KUNG’ANG’ANIA FILAMU NA MUZIKI PEKEE

 Mkurugenzi wa Idara ya Mfuko na Uwezeshaji kutoka BASATA Charles Ruyembe akifafanua masuala mbalimbali kuhusu Sekta ya Ubunifu na mchango wake katika ajira wakati akiwasilisha mada kwenyeJukwaa la Sanaa wiki hii.

 Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego akiieleza Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 na jinsi inavyofanya kazi zake hapa nchini kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii. Aliwataka wasanii kuacha kukimbilia sanaa za filamu na muziki pekee kwani kuna sanaa nyingine nyingi.

 Mwenyekiti wa Chama cha Sanaa za Maonesho Tanzania (CHASAMATA) Nkwama Ballanga akisisitiza jambo kwenye Jukwaa la Sanaa.

 Rais wa Shirikisho la Sanaa za Maonesho Tanzania Agnes Lukanga naye hakuwa nyuma katika kuchangia mada. Aliwakumbusha wasanii umuhimu wa kurudi darasani na kujijengea weledi.

Sehemu ya wadau waliohudhuria kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii wakifuatilia kwa makini programu.

Na Mwandishi Wetu

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeeleza kusikitishwa na hali iliyopo sasa ya wasanii kuzipa kisogo Sanaa zingine na kung’ang’ania filamu na muziki pekee hali inayowafanya wengi wao kubaki wakihangaika na kulalama.


Akizungumza wiki hii kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika makao makuu ya Basata, Katibu Mtendaji wa BASATA Ghonche Materego alisema kuwa, ni jambo la kushangaza kuona wasanii wakifunga milango yote katika sekta ya Sanaa na kubaki wakihangaika na madirisha mawili tu ya filamu na muziki.


“Ndugu zangu hebu tujiulize tu, Sanaa ni pana sana na ina fursa nyingi katika kutupa ajira na kuzalisha kipato kwa vijana wengi lakini kwa nini wote tunang’ang’ana na filamu na muziki pekee? Fursa nyingine tunamwachia nani? Alihoji Materego.


Alisema kuwa, tatizo lililopo sasa ni kwa vijana kusukumwa na fedha tu badala ya msukumo wa kisanaa hali ambayo imezifanya Sanaa zingine hususan za maonesho na ufundi kupigwa kumbo kutokana na matunda yake kuhitaji muda mrefu na juhudi.


Kwa mujibu wa Materego, ni wakati sasa wa Wasanii kufungua fursa walizozifunga katika fani nyingine za Sanaa vinginevyo haitawezekana kwa wasanii wote kutegemea milango ya filamu na muziki pekee katika kujiajiri bali fikra tofauti zinahitajika


“Haiwezekani tutegemee filamu na muziki pekee, hatutafika. Ni lazima tugeukie fursa zingine katika Sanaa. Sekta yetu ni pana na ina fursa nyingi sana ambazo zimekaa tu zinatusubili. Sisi ndiyo tutazifanya zipendwe na zituingizie kipato” alisisitiza Materego.


Kuhusu wasanii kujitokeza katika masuala mbalimbali yanayowahusu, Materego alisema, kumekuwa na tatizo ambapo katika makongamano, semina na mikutano mbalimbali wasanii wanayoitwa wamekuwa wakijitokeza kwa uchache au kutokuonekana kabisa.


“Mambo mengi yanajitokeza kuhusu wasanii na sekta ya Sanaa kwa ujumla, wasanii wetu wamekuwa wazito sana kushiriki. Hili nalo ni tatizo ni lazima tubadilike tujitokeze katika mambo yote yanayotuhusu” alieleza Materego.


Awali akiwasilisha mada kuhusu Tasnia ya Ubunifu na Mchango wake katika Ajira nchini, Mkurugenzi wa Idara ya Mfuko na Uwezeshaji kutoka BASATA, Charles Ruyembe alisema kuwa, muda umefika sasa wa somo la Sanaa kuanza kufundishwa mashuleni na kutahiniwa kama masomo mengine kwani kwa sasa ni fani inayoajiri vijana wengi.

No comments: