Mwasilishaji wa mada katika
jukwaa la Sanaa bwana Chediel Senzighe akisisitiza jambo wakati akitoa
mada kwenye kongamano la Jukwaa la sanaa, jijini Dar es Salaam jana.
Katibu Mkuu wa Chama cha
Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni Tanzania (CAJAtz) Hassan
Bumbuli akizungumza katika Kongamano la Jukwaa la Sanaa hapo jana.kulia
ni msanii Chediel Senzighe aliyekuwa muwasilishaji mada katika kongamano
hilo.
Na Mwandishi Wetu
Kongamano la Jukwaa la Sanaa ambalo huendeshwa kila wiki,
jana lilianza kwa kumkumbuka Mwandishi wa Habari na mwakilishi wa Kituo cha Channel
Ten, Daud Mwangosi aliyefariki dunia juzi katika vurugu zilizotokea katika
kijiji cha Nyololo mkoani Iringa.
Kabla ya kuanza kwa kongamano hilo jana, Mwendeshaji wa kongamano
hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na
Utamaduni nchini, (CAJAtz) Hassan Bumbuli aliwataka washiriki kusimama kwa dakika moja kumkumbuka
mwandishi huyo ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa
wa Iringa.
Katika kongamano hilo ambalo jana lilijadili mada ya Sanaa za jukwaani na guvu yake katika kufikisha ujumbe kwa
hadhira, mwasilishaji wa mada hiyo
Chediel Senzighe kutoka kundi la Jakaya Theatre, aliwakata wasanii kuandaa kazi
kwa kuzingatia maadili na kanuni ili
kuepusha kuipotosha jamii.
“Sanaa ina nguvu sana katika kufikisha ujumbe, kama ni
muuaji basi sanaa inauwezo wa kuua watu wengi kwa wakati mmoja, daktari akikosea
katika upasuaji ataua mgonjwa mmoja, lakini maudhui ya kazi ya sanaa yakikosewa
yanaathari kwa watu wengi na kwa wakati mmoja. Sasa ni vyema wasanii tukawa
makini katika kuandaa kazi zetu na zaidi tufanye utafiti kabla hatujaamua
kuandaa maudhui ya kazi zetu,” amesema Senzighe.
Wakichangia mada hiyo, washiriki wa kongamano hilo wamesema
tatizo kubwa linalowakabili wasanii siku hizi ni uvivu wa kusoma na kujifunza
na ndiyo maana wanaandaa kazi za kulipua huku akili zao zikiwaza fedha zaidi
kuliko kufikiria wanachokipeleka kwa jamii kinaweza kuleta athari gani.
“Wasanii wetu lazima wabadilike sasa, wafanye utafiti kabla
ya kuandaa sanaa hasa sanaa za jukwaani
au filamu hii itasaidia sana kuandaa maudhui mazuri ambayo pia yataisaidia jamii,”
amesema Godfrey Lebejo Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, mafunzo na habari wa
BASATA.
Awali wakati akifungua kongamano hilo, Katibu Mkuu wa
CAJAtz, bwana Bumbuli, alieleza kusikitishwa na kifo cha kinyama kilichomtokea
Mwandishi wa Channel Ten na kusema matumizi ya nguvu kupita kiasi ya jeshi la
Polisi yanahitaji kukomeshwa mara moja hasa kwa kuwa yanagharimu maisha ya watu
bila sababu za msingi.
“Inatusikitisha kama wanatsnia ya habari na kama Watanzania,
nguvu za polisi zinaacha majereha makubwa kwa watu na sasa zinagharimu maisha
ya watu, nguvu hizi hazina sababu na lazima zikemewe na kulaaniwa kwa nguvu
zote,” amesema Bumbuli.
No comments:
Post a Comment