ONYESHO la Usiku wa Sauti na Marafiki kweli ambalo
litakaowakutanisha wanamuziki mbalimbali waliowahi kupigia bendi ya Diamond
Sound ‘Dar es Salaam Kibinda Nkoi’ pamoja na wanamuziki wengine nyota nchini
utafanyika mwezi ujao.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Endless Fame
inayoandaa onyesho hilo, Zulfa Msuya amesema mjini Dar es Salaam kuwa,
kusogezwa mbele kwa onyesho kumetokana na baadhi ya wanamuziki kuwa safarini
huku wengine wakiwa katika kazi ya kurekodi na bendi zao.
“Tumelazimika kusogeza mbele onyesho hili kwa
sababu walengwa wakuu walikuwa safarini, wengine walikuwa wana kazi ya
kurekodi, kwa hiyo hawakuweza kuanza mazoezi kwa muda uliotakiwa, lakini sasa
wamesharejea wote na wako tayari kuanza kambi kwa ajili ya siku hiyo,” amesema.
Zulfa amesema wanamuziki hao watakuwa wakifanya
mazoezi katika ukumbi wa Princess Hall pale Sinza, Mapambano na mazoezi hayo
yatachukuwa wiki mbili.
Naye kiongozi wa Diamond Sound, Ibonga Katumbi
‘Jesus’ amesema wanataka kufanya onyesho ambalo litakuwa historia, hivyo bila
timu yote kukamilika isingekuwa rahisi wao kuanza mazoezi.
“Sisi hatujakaa pamoja zaidi ya miaka 12, ili
kupata muziki wenye kiwango cha juu ni lazima tukae si chini ya wiki mbili
kufanya mazoezi, ili watu wasikie ladha ile ile waliyokuwa wakisikia TCC,
Silent Inn.
“Wasisahau kuwa tutapiga pia nyimbo za Beta
Musica, sasa mtu kama Adolph hakuwepo Beta, Kata Nyama amepiga Beta wimbo
mmoja, lakini kuna wanamuziki kaka zetu watakuwepo pia nyimbo zao ni za miaka ya
1980 huko nao lazima zifanyiwe mazoezi, tuko makini kuhakikisha tunafanya hili
kwa ufanisi mkubwa,” amesema.
Jesus amesema kuanzia wiki ijayo utaratibu wa muda
wa kuanza mazoezi, ukumbi na matangazo mengine mbalimbali yataanza kutoka kwa
nguvu kwenye vyombo vya habari. Ameongeza pia kuwa hata nyimbo zingine zitaanza
kusikika katika mapigo tofauti lakini zikiimbwa na wanamuziki wote wa zamani.
No comments:
Post a Comment