USIKU WA SAUTI NA MARAFIKI WA KWELI
Ni moto Liva Hassan vs Alain Mulumba
MAMBO yameendelea kunoga katika usiku wa Sauti na Marafiki wa Kweli ambapo wanamuziki wa zamani wa bendi ya Diamond Sound wanatarajia kukutana, baada ya repa mwingine wa kiwango cha juu, Liva Hassan ‘Sultan’ kuthibitisha uwepo wake siku hiyo.
Kiongozi wa kundi hilo, Ibonga Katumbi ‘Jesus’ amesema tayari wamewasiliana na Liva Hassan na amekubali kuungana na ndugu zake katika siku hiyo kubwa ambayo itawakutanisha wasanii hao pamoja baada ya zaidi ya miaka 13.
“Liva atakuwa na sisi pale Princess Hall, sasa unaweza kupata picha mambo yatakuwaje, hapa Liva hapa Alain Mulumba, watu wanaweza kukumbuka mambo ya kupanda Kilimanjaro, kushuka Mount Meru, nawahakikishia watu wote onyesho hili litakumbusha kumbukumbu zetu nyingi,” amesema.
Jesus amesema kuongezeka kwa Liva kunafanya kikosi cha awali cha Diamond kubakiza wanamuziki wanne ambao walikuwa kwenye kikosi hicho cha kwanza kabisa ingawa pia wataongeza wanamuziki wengine wachache ambao walikuwa kwenye kundi la mwisho la Diamond ambalo lilirekodi kibao cha Valentine Day ambacho ulikuwa utunzi wake Mulumba.
“Jumatatu tutakutana wanamuziki wote, pale Kijitonyama, baada ya hapo mambo mengi zaidi yataendelea kusikika kwenye vyombo vya habari na hata wadhamini watasikika kuanzia wiki ijayo,” amesema.
Usiku huo unatarajia pia kupambwa naye Mhina Panduka, atakayeimba nyimbo zake mbalimbali za zamani na mpya na wanamuziki wengine wakongwe maarufu wa Tanzania.
Katika usiku huo, nyimbo kama Neema, Jetou, Chance, Mugheni, Seberne, Valentine Day, Infarouge maarufu kama Omari mbona unajikuna, na pia baadhi ya nyimbo za Beta Musica zitapigwa usiku huo.
No comments:
Post a Comment