Janeth Isinike
Lilian Tungaraza 'Internet'
WALIOKUWA wanenguaji wa mwanzo wa bendi ya Diamond Sound ‘Ikibinda Nkoi’ Janeth Isinike, Modesta Scud na Lilian Internet wanatarajia kujumuishwa katika kikosi kitakachotumbuiza kwenye onyesho la Usiku wa Sauti na Marafiki wa Kweli.
Akizungumza mjini Dar es Salaam, aliyekuwa Kiongozi wa Diamond Sound, Ibonga Katumbi ‘Jesus’amesema watawaita wanenguajia hao ili kuonyesha mshikamano baina yao kwani walifanya kazi nzuri pamoja na haitakuwa vyema kuwaacha.
“Sisi ni familia, kama familia lazima tuwe pamoja, mimi nimewaita wenzangu nifanye nao kazi pamoja, ni kama siku yangu ya kuzaliwa, Modesta, Janeth, Salima Abeid na Marehemu Elly Longomba waliweka historia pia katika unenguaji kwenye nchi hii.
“Baadaye wakaja kina marehemu Diana Aston Villa, Lilian Internet, Mamii Korando, wote waliibeba Diamond, sasa tutawaita Internet, Korando, Janeth na Modesta waungane na kaka zao wakati tunakutana Marafiki wa Kweli na tukionyesha sauti zetu,” amesema.
Lilian kwa sasa yupo Mashujaa Musica, Janeth ni mwimbaji wa African Stars ‘Twanga Pepeta’, Korando yuko Twanga wakati Modesta ameacha shughuli za unenguaji.
Jesus amesema mazoezi rasmi kwa ajili ya usiku huo ambao utakuwakutanisha wanamuziki hao baada ya miaka 14 yataanza Oktoba 15 pale katika ukumbi wa Princess uliopo Sinza Mapambano.
Wanamuziki ambao wamethibitisha kuwepo kwenye onyesho hilo ni Wayne Zola Ndonga, Richard Mangustino, Alain Mulumba ‘Kashama’, Elly Chinyama, Adolph Mbinga, Marcis Mengi, Kata Nyama, Andrew Sekidia, Hamza Waninga.
Mbali na hao waliokuwa Diamond Sound, onyesho hilo pia litamhushisha mwanamuziki mwingine maarufu nchini Mhina Panduka ‘Toto Tundu’ ambaye ataimba pia nyimbo zake mbalimbali zilizotamba zamani.
Diamond Sound ilitamba na nyimbo kama Jetou, Neema, Mgheni, Chance, Seberne na baadaye Kimalumalu. Katika onyesho hilo pia zitapigwa nyimbo za Beta Musica ambayo ilizaliwa baada ya kina Jesus, Mangustino, Chinyama kujitoa Diamond Sound.
No comments:
Post a Comment