22.11.13

Wednesday, May 29, 2013

(News) CHAMA CHA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA TANZANIA (TUMA)

Chama cha muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania (TUMA), kimepokea kwa majonzi na masikitiko makubwa taarifa ya msiba wa mwanamuziki maarufu na mashuhuri nchini Albert Mangwea (Ngwair) aliyefariki jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini jana.
Mwenyekiti wa TUMA nchini, Fredrick G Mariki (Mkoloni) ametoa salamu hizo za pole kwa familia ya marehemu Mangwea, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na mashabiki wa Bongo Fleva waliopo ndani na nje ya nchi kutokana na kuondokewa kwa msanii maarufu Albert Mangwair.
Marehemu Albert Mangwea ambaye alikuwa nchini Afrika Kusini kwa shughuli za kimuziki alifikwa na mauti hayo huku akiwa amelala katika chumba ambacho alikuwa na rafiki yake aliyetambulika kwa jina la M to The P ambaye naye alikimbizwa Hospitali ya St Helen iliyopo nchini Afrika Kusini kwa matibabu huku taarifa kamili ya kilichosababisha kifo cha Mangwea kikiwa bado hakijajulikana mpaka hapo Hospitali hiyo itakaposema.
“kwa niaba ya wanachama wa TUMA na Watanzania wote kwa ujumla napenda kutoa salamu za pole kwa familia ya marehemu Albert Mangwair kutokana na pigo hili kubwa na kwa kweli tumepoteza msanii wa kizazi kipya ambaye Taifa lilikuwa likijivunia kuwepo kwake na kazi zake” alisema Mkoloni.
Chama cha TUMA kinaungana na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu na kinatoa ushirikiano wa hali na mali kama ambavyo kimekuwa kikifanya hivyo katika mambo mengine yanayohusu wasanii nchini.
Mkoloni alimaliza kwa kusema kuwa “ni kweli tulimpenda lakini Mungu alimpenda zaidi na kuongeza kuwa ni wakati mgumu na tunatakiwa kushirikiana kwa pamoja katika kipindi hiki huku akitoa angalizo kwa watu wanaotaka kutumia fursa hii kwa ajili ya maslahi yao binafsi.

No comments: