22.11.13

Thursday, May 23, 2013

(News) Ethiopian Airline wadhamini wa usafiri wa Anga ZIFF 2013 na Skylight Band Kutumbuiza

 Kampuni ya usafiri wa anga.. Ethiopian airlines imejitokeza kudhamini Tamasha la 16 la filamu Tanzania, ZIFF linalotazamiwa kufanyika Zanzibar, June 29 hadi July 7, 2013. Meneja na Mkurugenzi msaidizi wa Tamasha hilo Daniel Nyalusi maarufu kwa kifupisho cha Dean alisema wanajisikia furaha sana kushirikiana na Kampuni hiyo, na kwamba anatarajia ushirikiano huo utafungua njia kwa makampuni mengine.

Aidha Dean alisema Ethiopian Airlines ndio wamekuwa wadhamini rasmi wa usafirishaji  wa watengenezaji filamu na wageni wote wa ZIFF kimataifa na kuongeza kuwa Tamasha la ZIFF 2013 linatarajiwa kufana zaidi kutokana na maandalizi yake na udhamini huu mkubwa wa Ethiopian Airline.
Pamoja na Ethiopian Airlines kampuni nyingine iliyojitosa kwenye udhamini wa Tamasha hilo ni ZUKU TV, hii itakuwa mara ya pili kampuni hii kushiriki katika kuunga mkono  Tamasha hilo, ambalo kwa miaka 16 iliyopita limesherehekea  kazi za sanaa nchini na kuwezesha uzalishaji wa filamu hapa Tanzania na duniani kote.
Akizungumziaa  ushirikiano huo,  Meneja wa ZIFF, Daniel Nyalusi alisema “ ZUKU inadhamini dola laki moja kila mwaka kwa miaka 10 kuanzia mwaka jana na itaangalia jinsi ya kupanua udhamini wake kadri muda unavyoendelaDean alisema “Tunakaribisha wadhamini wengine kushirikiana na ZIFF na matumaini yetu ni kwamba wadhamini wataweza kufaidika kutokana na ushirikiano huu  kwani ni nguzo ya masoko ya ubunifu kwa ajili ya wawekezaji na wafanyabiashara ambao wana maono kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na ajira katika sekta zote, hasa utalii na burudani.  Kwa kazi ya kukuza sekta ya burudani, ZIFF na Makampuni shiriki yatasaidia kujenga ajira kwa watengenezaji wa filamu, wazalishaji na watendaji katika kanda nzima.” Tamasha la ZIFF hupokea wageni zaidi ya 6000 toka nje kila mwaka na zaidi ya watu 45,000 wakati likiendelea Zanzibar.

SKYLIGHT BAND KUTUMBUIZA ZIFF
Bendi iliyokuja kwa kasi na inayoendelea kutamba hapa nchini kwa sasa Skylight Band inatazamiwa kuwa kivutio kikubwa katika tamasha la filamu nchini ZIFF.
Bendi hiyo inayoongozwa na mwanadada Aneth Kushaba, AK 47 inajipanga kupiga shoo kali ya karne katika Tamasha hilo la 16 la filamu za kimataifa litakalofanyika ndani ya Ngome Kongwe mjini Zanzibar.
Akizungumzia ushiriki wao Aneth Kushaba alisema “Zanzibar patakuwa hapatoshi, tumefurahi kupata fursa ya kutumbuiza ZFF na tunasubiri kwa hamu kubwa kujitangaza kimataifa”.
Skylight inayoundwa na wanamuziki kama Sam Machozi, Jonicho Flower na wengine kibao pia kwa sasa inatamba na vibao kama Karolina, Wivu, Nasaka Dough, na wimbo wao mpya Mbeleko.

No comments: