22.11.13

Tuesday, August 13, 2013

(News) Vodacom yazipiga jeki timu za Wawakilishi Zanzibar

 Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Ali Abdalla Ali (mwenye kofia)akipokea msaada wa vifaa vya michezo kutoka kwa Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Salum Mwalim kwa ajili ya timu ya mpira wa miguu na wa pete za Baraza la wawakilishi. Vodacom imezipatia timu hizo jezi, suti za michezo, viatu na mipira vikiwa na thamani ya Sh 4.5Milioni. Wanaoshuhudia ni Meneja wa timu Nassor Salum Aljazera(kushoto) na Meneja wa Vodacom Zanzibar Mohamed Mansour.

 Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Ali Abdalla Ali (mwenye kofia)akipokea mipira ya soka na pete  kutoka kwa Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Salum Mwalim kwa ajili ya timu za baraza la wawakilishi. Vodacom imezipatia timu hizo jezi, suti za michezo, viatu na mipira vikiwa na thamani ya Sh 4.5Milioni.

 Kutoka kushoto: Meneja wa Timu za Baraza la Wawakilishi Nassor Salum Aljazeera, Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Salum Mwalim, Naibu Spika wa Baraza la Wawakalishi Ali Abdala Ali, Meneja wa Vodacom Zanzibar Mohamed Mansour, Makamu mwenyekiti wa Michezo Baraza la Wawawakilishi Mbarouk Mtando na Mweka Hazina wa Baraza Dau Maulid kwa pamoja wakionesha vifaa vya michezo vilivyotolewa na Vodacom kusaidia timu za baraza.

 Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Salum Mwalim akiteta jambo na Naibu Spika wa Zanzibar Ali Abdala Ali na Meneja wa Timu za Baraza la wawakilishi Nassor Salum Aljazeera ambae pia ni Mwakilishi wa jimbo la Rahaleo wakati wa hafla fupi ya kupokea vifaa vya michezo vilivtolewa na Vodacom kusaidia timu ya soka na mpira wa pete za Baraza.

 Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Salum Mwalim akiongea wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa vya michezo vilivyotolewa na Vodacom kwa timu za Baraza la Wawakalishi iliyofanyika ofisi za Baraza hilo Mjini Zanzibar. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haji Omar Kheri na Naibu Spika wa Zanzibar Ali Abdalla Ali. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haji Omar Kheri akiongea wakati wa hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa vya michezo vilivyotolewa na Vodacom kwa timu za Baraza la Wawakalishi iliyofanyika ofisi za Baraza hilo Mjini Zanzibar. Wengine pichani ni Naibu Spika wa Zanzibar Ali Abdalla Ali(katikati) na  Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Salum Mwalim.

Kampuni ya Vodacom Tanzania imekabidhi vifaa mbalimbali vya michezo kwa ajili ya timu za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ili kuzipiga tafu timu hizo kushiriki kwenye mashindano ya urafiki mwema yanayotarajiwa kufanyiaka jijini Arusha mwishoni mwa mwezi huu.
Vifaa hivyo ambavyo ni seti mbili za jezi kwa kila timu ya soka na ya mpira wa pete, mipira, viatu, soksi na suti za michezo vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh 4 Milioni vimepokelewa leo na Naibu Spika wa Zanzibar Ali Abdala Ali kwenye hafla fupi iliyofanyika ofisi za Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Akipokea vifaa hivyo Naibu Spika Ali ameishukuru Vodacom kwa msaada huo alioutaja kuwa ni silaha nzuri itakayoziwezesha timu za Baraza kushiriki vema na kwa kujiamini kwa kile alichokifananisha na nondo kwenye ujenzi wa nyumba.
“Vodacom mmetupatia nondo za michezo kwa kuwa kama ilivyo kwenye ujenzi wa nyumba nondo ni kifaa muhimu vivo hivyo nondo za kwenye michezo ni vifaa bora hivyo hatuna budi kuwashukru (Vodacom) kwa dhati kabisa kwa msaada huu.”Alisema Naibu Spika
Naibu Spika Ali amesema timu za Baraza la Wawakilishi zimekuwa kwenye uhitaji wa vifaa kuhakikisha inakuwa na ushiriki mzuri kwenye mashindano mbalimbali ikiwemo ya hivi karibu ambayo ni ya Arusha itakayoshirikisha timu mbalimbali zikiwemo za Mabunge pamoja na mashindano ya maadhimisho ya miaka hamsini ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema msaada huo sio tu kwamba umelifurahisha Baraza la Wawakilishi bali Serikali na Wazanzibari wote kwa ujumla kwa kuwa unaonesha muendelezo wa kazi nzuri na kubwa inayofanywa na Vodacom katika kusaidia jamii hapa Zanzibar.
“Tumefarijika sana na msaada huu tumekuwa mashuhuda na wenye kusikia kazi za kijamii mnazozifanya hapa Zanzibar na leo mnageukia michezo hili linamfurahisha kila mmoja na kwa niaba ya Baraza na wadau wengine wote tunawashukuru.”Alisema Naibu Spika na kuongeza kuwa “Mmetuwezesha kwenda Arusha na sasa tunawaomba (Vodacom) muangalie jinsi mtakavyoweza kusaidia timu zetu hizi na maeneo mengine tunapoelekea kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.”
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haji Omar Kheri ambae pia ni Mwenyekiti wa Wawakilishi Sports Club amesema Zanzibar inatambua kazi kubwa Vodacom inayofanya kusaidia jamii na hivyo kuifanya kampuni hiyo kuwa moja ya kampuni kubwa zaidi hapa nchini.
Vodacom ni moja ya kampuni kubwa za kibiashara hapa nchini mmejiunga vizuri na mmekuwa na kazi nzuri za kuboresha huduma zenu lakini kipekee tunafurahishwa na kazi zenu za kusaidia jamii hapa nchini……. Na kwa upande wa hivi vifaa tumevipokea kwa furaha kubwa”
Akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa hivyo Meneja wa Uhusiano wa Nje wa Vodacom Salum Mwalim amesema Vodacom inatambua nafasi ya viongozi wa kitaifa wakiwemo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika kushajiisha ajenda za maendneleo ikiwemo michezo.
Mwalim amesema kuwa Vodacom inaamini kuwa kasi ya ushiriki wa Wawakilishsi kwenye michezo ni chachu katika kuinua kiwango cha michezo mjini Zanzibar.
“Vodacom tunatambua umuhimu wa nyie (Wawakilishi)kushiriki katika michezo jamii inapowaona mkiwa katika mstari wa mbele kwenye michezo bila shaka nao wanahamisika na kushiriki michezo na kwa njia hiyo basi tunajenga afya zetu, tunaimarisha udugu na mshikano na kujenga urafiki na nchi za nje.”Alisema Mwalim
“Kote mtakapopita kuelekea Arusha wananchi watawaona na kupitia kwenu ujumbe wa michezo utaenea na hivyo kuendeleza michezo.”Alisema
Kazi ya kukuza michezo haiwezi kuachwa kwa Serikali na ZFA (Chama Cha Soka Zanzibar) pekee ila ni jambo linalohitaji wadau kujitokelea na kutumia utashi wa kisiasa wa michezo mlionao kuisadia Serikali na ZFA kurudisha enzi tukufu za michezo zilizowahi kuwika Zanzibar katika miaka ya themanini na tisini.”Aliongeza Mwalim
Mwalim ameziomba timu za Wawakilishi kutumia msaada huo kama chahu ya kufanya vema na kurudi na ushindi kutoka mashindano ya Arusha huku pia ikijipanga vema kwa mashindano ya maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibaryatakayozishirikisha timu za mabunge ya Afrika Mashariki.
Mwisho.

No comments: